Jumamosi 1 Novemba 2025 - 16:27
Kwa nini Imam Mahdi (a.t.f.) anaitwa “Shariki al-Qur’an” (Mshirika wa Qur’ani)?

Hawza/ Maana ya kina ya neno “Sharik al-Qur’an” (mshirika wa Qur’ani) inaashiria uhusiano wa kudumu kati ya Imam Mahdi (aj) na Qur’ani Tukufu katika kuendeleza uongofu, kuifufua dini, na kulinda ukweli wa wahyi wa Mwenyezi Mungu.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, jina lenye nuru “Sharik al-Qur’an” linaonesha uhusiano usiokatika kati ya Imam Mahdi (a.t.f.) na Qur’ani Tukufu — uhusiano ambao ndio siri ya kudumu kwa uongofu wa kimungu na uhai wa kiroho kwa Uislamu katika zama za ghaiba.

Kumuarifisha Imam Mahdi (a.s.) kwa tamko hili tukufu na lenye heshima “Sharik al-Qur’an” kunatokana na maneno ya Maimamu watoharifu (a.s.). Tafsiri hii imetajwa katika baadhi ya ziara mashuhuri, zikimsemesha Imam Husayn (a.s.) na Imam Mahdi (a.s.):

«السَّلامُ عَلَیْکَ یا أَمینَ الرَّحْمانِ، السَّلامُ عَلَیْکَ یا شَرِیکَ القُرآن.»

Amani iwe juu yako, ewe mlinzi wa rehema za Rahman; amani iwe juu yako, ewe mshirika wa Qur’ani. (1)

«السَّلامُ عَلَیْکَ یا صاحِبَ الزَّمانِ، السَّلامُ عَلَیْکَ یا خَلیفَةَ الرَّحْمانِ، السَّلامُ عَلَیْکَ یا شَرِیکَ القُرآنِ، السَّلامُ عَلَیْکَ یا قاطِعَ البُرْهان.»

Amani iwe juu yako, ewe Bwana wa zama; amani iwe juu yako, ewe khalifa wa Rahman; amani iwe juu yako, ewe mshirika wa Qur’ani; amani iwe juu yako, ewe mwenye hoja thabiti. (2)

Kadhalika, kwa kuwa neno “Shurakā’ al-Qur’an” (washirika wa Qur’an) limetumika katika ziara zinazowahusu Maimamu wote (a.s.), bila shaka umbo lake la umoja — “Sharik al-Qur’an” — linamhusu hasa yule mhimili wa mwisho wa mlolongo wa uongozi huu mtukufu, yaani Imam Mahdi (a.s.):

«السَّلامُ عَلَیْکُمْ أَئِمَّةَ الْمُؤْمِنِینَ ... وَشُرَکاءَ الْفُرْقانِ وَ مَنْهَجَ الْإِیمان.» (3)
«السَّلامُ عَلَیْکُمْ أَئِمَّةَ الْمُؤْمِنِینَ وَ سادَةَ الْمُتَّقِینَ ... وَ شُرَکاءَ القُرآن.» (4)

Kwa hivyo, kuwa Sharik al-Qur’an humaanisha kuwa sambamba na Qur’ani — jambo lililotajwa wazi katika hadithi mashuhuri ya Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) aliposema:

«إِنِّی تَارِکٌ فِیکُمُ الثَّقَلَیْنِ، کِتابَ اللّٰهِ وَعِتْرَتِی، ما إِنْ تَمَسَّکْتُمْ بِهِما لَنْ تَضِلُّوا أَبَداً.»

“Nimewaachieni mambo mawili mazito: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu (Ahlul-Bayt). Mkishikamana navyo vyote viwili, kamwe hamtapotea.”  (5)

Kwa kuwa Ahlul-Bayt (a.s.) wametajwa kuwa wenza na washirika wa Qur’ani, basi katika zama hizi, maana hiyo imejidhihirisha kwa ukamilifu kwa mtukufu pekee aliye baki miongoni mwao — Imam Mahdi (a.s.). Yeye ndiye aliye pamoja na Qur’ani na daima atasimama sambamba nayo.

Kwa hiyo, ili Umma wa Kiislamu udumishe amana za Mtume wake, ni lazima ushikamane na Qur’ani pamoja na kushikamana na uongozi wa Sharik al-Qur’an, Imam Mahdi (a.s.).

Endapo dhana ya Sharik al-Qur’an kwa Imam (a.s.) itawekwa sambamba na dhana ya Sharik al-Imam kwa Qur’ani — ikimaanisha ushirika wa Qur’ani na Imam katika nyanja zote za muujiza na uongofu — basi maneno ya Mtume (s.a.w.w.) yanabaki kuwa mwongozo kamili:

“Mtakaposhikamana na vyote viwili, hamtapotea kamwe.”

Kushikamana na Qur’ani kunakuwa na matokeo halisi pale kunapoambatana na kushikamana na Imam Mahdi (a.s.), na vivyo hivyo — kushikamana na Imam (a.s.) kunakuwa na nguvu pale kunapounganishwa na Qur’ani.
Pindi Qur’ani na Imam watakapochukuliwa kwa pamoja katika maisha ya mtu au jamii, uongofu wao unakuwa ni wa uhakika; lakini pindi wote wawili watakaposahauliwa, matokeo yake ni upotovu na anguko.

Ikiwa Imam atatajwa bila Qur’ani, au Qur’ani itatajwa bila Imam (a.s.), basi nafasi ya uongofu wa wote wawili itakuwa dhaifu, na hautazaa matunda ya kiroho na kimaadili.

Mfano wa ushirikiano huu unaweza kuelezwa kama uhusiano wa maji na jua katika kukuza mmea: mmea hukua kwa ushirikiano wa vyote viwili; bila jua, unakufa kwa unyevunyevu, na bila maji, unateketea kwa joto.

Kwa mtazamo huu wa kipekee wa ushirikiano kati ya Qur’ani na Imam, tunaweza kusema kuwa; katika mantiki ya Mtume (s.a.w.w.), ambayo inalingana na wahyi wa kimungu, Qur’ani isiyo pamoja na Imam Mshirika (Sharik al-Imam) — ingawa itasomwa na kuhifadhiwa — haitakuwa “muujiza wa milele kwa Uislamu”. Itabaki kuwa ni kitabu, ni nakala ya wahyi, lakini haitakuwa Kitabu cha uongofu wala mwongozo wa furaha ya kweli. Kadhalika, Imam asiye Sharik wa Qur’ani ni Imam kwa jina, lakini si Imam ma‘sūm.

Ndiyo maana Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) alisema:

«عَلِیٌّ مَعَ القُرآنِ وَ القُرآنُ مَعَ عَلِیٍّ.»

Ali (a.s.) yuko pamoja na Qur’ani, na Qur’ani iko pamoja na Ali (a.s.). (6)

Na tukikubali kuwa Imam Ali (a.s.) na Imam Mahdi (a.s.), kama mwanzo na mwisho wa mlolongo wa wasii wa Mtume, ni mwanga mmoja katika sura mbili, basi tunaweza kupanua maneno hayo ya Mtume (s.a.w.w.) na kusema:

«المَهْدِیُّ، عَلَیْهِ‌السَّلامُ، مَعَ القُرآنِ وَ القُرآنُ مَعَ المَهْدِیِّ، عَلَیْهِ‌السَّلامُ.»

“Mahdi (aj) yupo pamoja na Qur’ani, na Qur’ani ipo pamoja naye.”

Kauli hii tukufu inaeleza kwa namna nyingine yale yaliyomo katika usemi wa kina wa “Shariiku al-Qur’an” — yaani kuwa Imam Mahdi ni mshirika wa Qur’ani Tukufu.

Iwapo “ushirika na Qur’ani” unahusiana na jukumu la Imam Mahdi (a.s) katika kuendeleza na kufufua uhai wa Qur’ani, basi tunapata dalili nyingi katika riwaya na ziyara mbalimbali, kama vile:

«اللّٰهُمَّ جَدِّدْ بِهِ ما امْتُحِیَ مِنْ دِینِکَ، وَأَحْیِ بِهِ ما بُدِّلَ مِنْ کِتابِکَ.»

“Ewe Mola, kwa kupitia yeye, vifufue vipengele vya dini Yako vilivyofutwa, na uhuisho yale yaliyobadilishwa kutoka katika Kitabu Chako.” (7)

«... وَ أَحْیِ بِوَلِیِّکَ القُرآنَ.»

“Na kwa kupitia walii Wako, uihuishe Qur’ani.” (8)

«وَ أَحْیِ بِهِ مَیِّتَ الْکِتابِ وَ السُّنَّةِ.»

“Ewe Mola, mfanye Imam Wako kuwa ni mhuishaji wa Qur’ani na Sunna ya Mtume Wako (s.a.w.w).” (9)

Kwa kuzingatia kwamba du’a na ziyara hizi zinatokana na kauli za Maimamu watoharifu (a.s), na baadhi yao hata zimepokelewa kutoka kwa Imam Mahdi (a.s) mwenyewe, zinaonesha wazi nafasi muhimu na ya kipekee ya Imam Mahdi (a.s) katika kuifufua Qur’ani na uhai wa mafundisho yake.

Hivyo basi, haya yote ni muonekano mwingine wa ukweli wa “Shariiku al-Qur’an”, yaani kuwa Imam Mahdi (a.s) ni mshirika wa Qur’ani katika uhai, ufasiri na utekelezaji wake.

Rejea:
1. Majlisi, Muhammad Baqir, Bihār al-Anwār, juzuu ya 97, uk. 336, Beirut.
2. Qummi, Shaykh Abbas, Mafātih al-Jinān, mlango wa Jāmi‘ al-Ziyārāt.
3. Majlisi, Bihār al-Anwār, juzuu ya 97, uk. 207.
4. Ibid., juzuu ya 99, uk. 163.
5. Kanz al-‘Ummāl, juzuu ya 1, uk. 44; Musnad Ahmad ibn Hanbal, juzuu ya 5, uk. 89 na 182.
6. Yanābī‘ al-Mawadda, uk. 90.
7. Ṣalawāt Abū al-Hasan Ḍarrāb Iṣfahānī.
8. Qummi, Shaykh Abbas, Mafātih al-Jinān, Ziyārat Imām al-Zamān (a.s).
9. Rejea hiyo iliyopita

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha